Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amefanya ziara rasmi ya siku mbili nchini Kenya kufuatia mwaliko wa mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta.
Akiwa Ikulu jijini Nairobi Mhe. Rais alifanya mazungumzo ya faragha na mwenyeji wake Mhe. Rais Kenyatta na baadaye walifanya mazungumzo rasmi ambayo yalihudhuriwa na wajumbe wa pande zote mbili.
Akizungumza mbele ya waandishi wa habari baada ya kumaliza mazungumzo yao Mhe. Rais Samia amesema wamekubaliana kukuza na kuimarisha uhusiano wa kiuchumi, kibiashara, kidugu, kihistoria na wa kirafiki uliopo baina ya nchi mbili.
Mhe. Rais Samia amesema kuwa wamekubaliana kutekeleza miradi ya pamoja ya kimkakati ikiwamo miradi ya usafiri na usafirishaji wa watu na bidhaa na kuangalia jinsi ya kupata nishati ya umeme na gesi kutoka upande mmoja kwenda upande mwingine ikiwa ni pamoja na ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi kutoka Dar es salaam hadi Mombasa na kusisitiza kuwa ni wakati wa kuitekeleza miradi hiyo kwa vitendo.
Mhe. Rais amesema kuwa wamekubaliana kuimarisha miundombinu ya usafirishaji kwa kujenga barabara, kuimarisha usafiri wa majini katika ziwa Victoria, reli na anga na kushughulikia uondoaji wa vikwazo vya biashara visivyo vya kodi na kuagiza Tume ya pamoja ya Ushirikiano (JPC) kukutana kushughulikia vikwazo hivyo ili kuondoa mivutano na misuguano inayokwamisha juhudi za kukuza uchumi kwa nchi hizo.
Amesema Tanzania imejipanga kwa nguvu zote kuwekeza nchini Kenya ili kukuza ujazo wa biashara na kuongeza miradi ya uwekezaji kutoka kampuni 30 za watanzania zilizowekeza mtaji wenye thamani ya Shilingi bilioni 19.3 za Kenya ambazo ni sawa na Shilingi bilioni 410.2 za Tanzania na kutoa ajira kwa wakenya 2640.
Amesema Kenya ni miongoni mwa nchi zilizowekeza nchini kwa kiwango kikubwa ambapo kampuni 513 za nchi hiyo zimewekeza nchini mtaji wenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.7 ambazo ni sawa na Shilingi trilioni 3,888 na kuzalisha ajira 51,000 kwa watanzania na amemuhakikishia mwenyeji wake kuwa atawashawishi wafanyabiashara na wawekezaji wa Tanzania kuwekeza kwa wingi nchini Kenya.