Tarehe 25 Septemba, 2021 Tanzania na Kenya zilifanikiwa kuondoa vikwazo 12 visivyo vya kikodi kati ya nchi hizo mbili.

Hatua hii imefikiwa katika Mkutano wa Kamati ya Pamoja ya Biashara kati ya Tanzania na Kenya uliofanyika tarehe 25 Septemba, 2021 katika hoteli ya Sarova Whitesands mjini Mombasa, Kenya. Mkutano huo uliongozwa kwa pamoja na Ndg. Dotto James, Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara Tanzania na Balozi Johnson Weru, Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda Kenya.

Balozi John Simbachawene, Balozi wa Tanzania nchini Kenya pia alihudhuria Mkutano huo akiambatana na Ndg. Mohammed Haji- Konseli Mkuu wa Tanzania mjini Mombasa.

Hatua hii ni muendelezo wa matokeo mazuri ya ziara ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan nchini Kenya mwezi Mei 2021 ambapo ilielekezwa kwamba taasisi husika upande wa Tanzania na Kenya zikutane ili kujadili na hatimaye kuondoa vikwazo vya biashara kati ya nchi hizi mbili.

Katika kuhitimisha mkutano huo, Balozi John Simbachawene, Balozi wa Tanzania nchini Kenya alieleza kwamba mafanikio haya yanapelekea Idadi ya vikwazo vilivyoondolewa kati ya Tanzania na Kenya kufikia 42 kutoka vikwazo 30 vilivyoondolewa kwenye Mkutamo uliofanyika mwezi Mei 2021 mjini Arusha, Tanzania.  Taratibu za kuondoa vikwazo 18 vilivyobakia  zinaendelea kwa pande zote mbili na inatarajiwa kwamba kufikia mwezi January 2022 vikwazo vyote vitakiwa vimepatiwa ufumbuzi.  

Balozi Simbachawene aliongeza kwamba kuendelea kuondolewa kwa vikwazo hivyo kunatoa fursa zaidi kwa Tanzania kufanya biashara na Kenya hivyo aliwakaribisha wafanyabiashara wa Tanzania kuendelea kuchangamkia fursa za biashara zilizopo kati ya nchi hizi mbili