Tarehe 24 Sept 2021, Mhe. Dkt. John S. Simbachawene, Balozi wa Tanzania nchini Kenya alishiriki mazungumzo kati ya Katibu Mkuu Wizara ya Viwands Tanzania, Ndg. Dotto James na Katibu Mkuu Viwanda- Kenya Balozi Johnson Weru katika kufanya maandalizi ya Mkutano wa Sita wa Biashara kati ya Tanzania na Kenya utakaofanyika tarehe 25 Septemba, 2021, Mombasa Kenya.

 Katika mazungumzo hayo, Viongozi hao walikubaliana kuendelea kuchambua vikwazo mbalimbali vya kibiashara vilivyopo kati ya Kenya na Tanzania na kuviondoa katika kutekeleza maelekezo waliyoyatoa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Uhuru Kenyatta, Rais wa Jamhuri ya Kenya mwezi Mei 2021.

Vilevile, Katibu Mkuu Viwanda Kenya aliipongeza Tanzania kwa kuridhia Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (ACfTA) mwezi Septemba, 2021 akieleza kwamba itatoa fursa nyingi za biashara kati ya Tanzania na Kenya na Afrika kwa ujumla. Hivyo makubaliano ya kuondoa vikwazo vya biashara kati ya Tanzania na Kenya yatachangia katika kuwezesha utekelezaji wa mkataba huo kwa nchi zote mbili kwa vile nchi hizi zinategemeana sana kibiashara.

Kwa upande wake, Balozi Dkt. John Simbachawene alimshukuru Katibu Mkuu Viwanda Kenya kwa kuitisha mkutano huo na kuahidi kwamba Ubalozi upo tayari kuendelea kushirikiana na Serikali ya Kenya na wadau wengine katika kutekeleza makubaliano yatakayofikiwa kwenye mkutano huo ili kuimatisha biashara kati ya nchi hizi mbili.

Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na Balozi Fatma.Rajab, Naibu Katibu Mkuu Wizara Mambo ya Nje - Tanzania, Ndg. Amina Shaaban, Naibu Katibu Mkuu Fedha na Mipango, Ndg. Mohammed Haji- Konseli Mkuu wa Tanzania mjini Mombasa na Ndg. Ally Gugu, Mkurugenzi wa Biashara Tanzania.

Itakumbukwa kwamba, Mkutano wa Tano wa Biashara kati ya Tanzania na Kenya ulifanyika mwezi Mei 2021, Arusha Tanzania na kufanikiwa kuondoa vikwazo 30 na kubakiza vikwazo 34 tu.