Ubalozi wa Tanzania nchi Kenya unapenda kuwapongeza Taasisi na Kampuni zote zilizoshiriki katika Banda la Tanzania na kuonesha umahiri mkubwa uliopelekea kupata Kombe la Banda Bora katika Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Nairobi (Nairobi International Trade Fair) yanayofanyika jijini Nairobi kuanzia tarehe 28 Septemba, 2026 na kuhitimishwa tarehe 4 Oktoba 2026. wageni wengi ikiwemo Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya Mifugo wa Serikali ya Jamhuri ya Kenya, Mhe. Mutahi Kagwe, waliotembelea banda la Tanzania, walivutiwa na ubora wa bidhaa mbalimbali pamoja na huduma zilizotolewa katika banda hilo, zikiwemo bidhaa za ngozi, asali na nafaka.

Chini ya uratibu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) na kampeni ya โ€œMade in Tanzaniaโ€ kampuni tatu za KOM Food Products, Woiso Original Products na Asilia African Honey zinazozalisha bidhaa chakula, ngozi na asali, mtawalia zilishiriki. Ushiriki wa TanTrade katika maonesho haya unalenga kutangaza bidhaa zinazozalishwa nchini Tanzania kupitia kampeni ya Made in Tanzania, kutafuta masoko na kuunganisha wazalishaji na fursa za biashara katika soko la ukanda wa Afrika Mashariki na Kimataifa.

Aidha, miongoni mwa taasisi nyingine zilizoshiriki masonesho hayo ni pamoja na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ambayo inatangaza miradi yake mbalimbali ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa jengo la ghorofa 22 linalojengwa jijini Nairobi kwa ubia na serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ya Tanzania.