Waziri wa Ujenzi, Mhe. Masanja Kungu Kadogosa, amesema Serikali ya Tanzania imejipanga kuimarisha utekelezaji wa miradi ya miundombinu kupitia mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (Public Private Partnership – PPP).
Mhe. Kadogosa ameyasema hayo jijini Nairobi, Kenya, wakati wa Kongamano la 16 la Bara la Afrika kuhusu Ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), ambapo amesisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kutumia mfumo huo kama njia mojawapo ya kuongeza uwezo wa kugharamia na kutekeleza miradi mikubwa ya miundombinu.
Amesema, kwa kuangalia uzoefu wa Kenya, Tanzania itaweza kubaini mifumo bora ya utekelezaji, namna ya kuvutia wawekezaji binafsi na kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza katika utekelezaji wa miradi hiyo.
Kongamano hilo limewakutanisha wadau kutoka mataifa mbalimbali, yakiwemo Kenya, Uganda, Ufaransa, Tunisia, Ivory Coast na Senegal, kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kujadili mikakati ya kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi katika kufadhili na kutekeleza miradi ya maendeleo barani Afrika.
Hatua hiyo inaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga uchumi shindani na jumuishi kupitia uwekezaji katika miundombinu ya kisasa, kuongeza ushiriki wa sekta binafsi na kuharakisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati kwa maendeleo ya Taifa.

